07/09/2026
“Saratani si hukumu ya kifo.” Huo ni ujumbe wa matumaini uliotolewa na Askofu Macha wakati wa uzinduzi wa Foundation yenye lengo la kuhamasisha jamii kuondokana na hofu ya saratani na kuzingatia elimu sahihi kuhusu ugonjwa huo.
Akizungumza katika hafla hiyo Askofu Macha alisisitiza umuhimu wa jamii kupata taarifa sahihi kuhusu saratani huku akieleza kuwa hofu na dhana potofu zinaweza kuwafanya watu kuchelewa kutafuta huduma za afya.
Alisema kuwa saratani inapogundulika mapema mgonjwa anaweza kupata nafasi nzuri zaidi ya kupata matibabu na kuendelea na maisha yake. Hivyo, alitoa wito kwa wananchi kutopuuza dalili zinazoweza kuashiria ugonjwa huo.
“Tusisubiri mpaka ugonjwa uwe mkubwa", ni msisitizo unaobeba ujumbe muhimu kwa jamii: uchunguzi wa afya kwa wakati unaweza kuwa hatua ya kwanza ya kuokoa maisha.
Uzinduzi huo pia umeendelea kuimarisha wito wa ushirikiano kati ya taasisi za afya, viongozi wa dini, wadau na jamii katika kutoa elimu, kuhamasisha uchunguzi na kupunguza unyanyapaa kwa watu wanaoishi na saratani.
Naye Mwanzilishi wa taasisi hiyo Lydia Mcharo ambaye alipata matibabu ya saratani na kupona katika Taasisi ya Saratani Ocean Road (ORCI) alisema kwa kuanzia taasisi hiyo itajikita katika mapambano dhidi ya saratani ya matiti na saratani ya mlango wa kizazi.
Lyidia alisema taasisi hiyo inalenga kuongeza uelewa wa jamii kuhusu umuhimu wa uchunguzi, kugundua saratani katika hatua za awali, kupata matibabu kwa wakati na kuwapatia wagonjwa msaada wanaohitaji katika safari ya matibabu.
Akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Saratani Ocean Road (ORCI) Dkt. Diwani Msemo,Daktari bingwa wa Magonjwa ya Saratani Dkt. Kandali Samweli alisema kuanzishwa kwa True Rehoboth Cancer Foundation ni hatua inayoongeza nguvu katika jitihada za Serikali na wadau mbalimbali katika mapambano dhidi ya saratani nchini.
Dkt. Kandali alisema Taasisi ya Saratani Ocean Road (ORCI) inapokea baadhi ya wagonjwa ambao wamefika katika hatua za juu za ugonjwa hali inayoweza kufanya matibabu kuwa na changamoto zaidi.