04/06/2026
WATUMISHI PSSSF WACHANGIA MILIONI 10 KWA MATIBABU YA WATOTO WENYE VICHWA VIKUBWA NA MGONGO WAZI MOI
Na Amani Nsello - MOI
Watumishi wa Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma (PSSSF) wamechangia kiasi cha shilingi milioni 10 kusaidia matibabu ya watoto wenye tatizo la vichwa vikubwa na mgongo wazi wanaopatiwa matibabu katika Taasisi ya Tiba ya Mifupa na Ubongo Muhimbili (MOI).
Mbali na mchango huo wa fedha, watumishi hao pia walikabidhi msaada wa mahitaji mbalimbali muhimu kwa watoto hao, ikiwemo miswaki, sabuni za unga, pampasi na maziwa, ikiwa ni sehemu ya kuunga mkono juhudi za kuboresha ustawi wao wakati wa matibabu.
Akizungumza wakati wa kukabidhi msaada huo jana Juni 03, 2026, Mratibu wa shughuli hiyo kutoka PSSSF, Bi. Maria Lupondo, amesema watumishi wa mfuko huo wameguswa na mahitaji ya watoto hao na kuona umuhimu wa kushiriki katika kuwasaidia ili kupunguza changamoto wanazokutana nazo wao na familia zao.
"Mchango huu unaakisi dhamira ya watumishi wa PSSSF ya kurejesha sehemu ya mafanikio yetu kwa jamii kwa kuwasaidia wenye uhitaji, hususani watoto wanaohitaji huduma maalumu za matibabu".
Kwa upande wake, Meneja wa Wagonjwa wa Ndani MOI, Magreth Kumpuni, ambaye alipokea msaada huo kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi hiyo, aliwashukuru watumishi wa PSSSF kwa moyo wao wa kujitolea na msaada walioutoa.
Amesema mchango huo utasaidia kuboresha huduma na mahitaji ya watoto wanaopatiwa matibabu katika taasisi hiyo, huku akizitaka taasisi na wadau wengine kuendelea kushirikiana na MOI katika kusaidia makundi yenye mahitaji maalumu ya kiafya.
Msaada huo ni sehemu ya juhudi za wadau mbalimbali zinazolenga kuimarisha huduma za afya na kuwapatia matumaini watoto wanaokabiliwa na changamoto za vichwa vikubwa na mgongo wazi nchini.